News

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUFUTWA KWA USAJILI WA KUDUMU WA VYAMA VITATU VYA SIASA

2016-11-09 13:04:38

Nachukua fursa hii kuutaarifu umma wa watanzania kuwa, kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992, nimefuta usajili wa kudumu wa vyama vya siasa vitatu vifuatavyo kuanzia leo 09 Novemba 2016:-

    1. Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA) kilichopata usajili wa kudumu tarehe 15 Novemba 2001, ambacho kilikuwa kinaongozwa na Bwana James Mapalala kama Mwenyekiti wa Taifa na Bi Mwaka Lameck Mgimwa kama Katibu Mkuu.

    2. Chama cha “The African Progressive Party of Tanzania “(APPT-Maendeleo)kilichopata usajili wa kudumu tarehe 4 Machi 2003 ambacho kilikuwa kinaongozwa na Bwana Peter Kuga Mziray kama Rais Mtendaji Taifa na Bwana Nziamwe Samwel kama Katibu Mkuu.

    3. Chama cha Jahazi Asilia kilichopata usajili wa kudumu tarehe 17 Novemba, 2004 kilichokuwa kinaongozwa na Bwana Kasimu Bakari Ally kama Mwenyekiti Taifa na Bwana Mtumweni Jabir Seif kama Katibu Mkuu.

Mchakato wa kufuta usajili wa vyama hivi unatokana na zoezi la uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika kuanzia tarehe 26 Juni mpaka 26 Julai, 2016.

Katika zoezi hilo la uhakiki ilibainika kuwa, vyama vya siasa tajwa hapo juu vimepoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa, hivyo kila chama kilipewa taarifa ya nia ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuta usajili wake wa kudumu na kutakiwa kueleza kwa nini kisifutwe. Katika utetezi wao vyama hivi vilishindwa kutoa sababu za kuridhisha kuwa havijakiuka sheria na bado vinazo sifa za usajili wa kudumu.

Mapungufu kwa ujumla wake ambayo yameonyeshwa kwenye kila taarifa ya kufuta usajili wa kudumu iliyopelekwa kwa chama husika, ni pamoja na yafuatayo:-

1.   Kutokuwa na ofisi ya chama Tanzania Bara na Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 10(d);

2.   Kutokuwa na wanachama Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 10(b);

3.   Kushindwa kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi ya chama kwa mujibu wa kifungu cha 14(1)(a);

4.   Kushindwa kuwasilisha hesabu zake za mapato na matumizi ya mwaka kwa Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili zikaguliwe kwa mujibu wa kifungu cha 14(1)(b)(i);

5.   Kushindwa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa tamko la orodha ya mali za chama kwa mujibu wa kifungu cha 14(1)(b)(ii); au

6.   Kushindwa kutekeleza matakwa ya kifungu cha 15(1) kwamba mapato yote ya fedha ya chama yawekwe katika akaunti ya chama.

 

Kwa mujibu wa kifungu cha 7(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, taasisi yoyote hairuhusiwi kufanya kazi kama chama cha siasa kama haijasajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Hivyo, nawakumbusha waliokuwa wanachama na viongozi wa vyama vya siasa ambavyo nimevifutia usajili wa kudumu kuwa, hawapaswi kufanya shughuli yoyote ya kisiasa kwa kutumia jina la chama cha siasa kilichofutwa.  Kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi, ikiwamo Sheria ya Vyama vya Siasa.

Pamoja na kufuta usajili wa kudumu wa vyama vya siasa hivi vitatu, pia naviasa vyama vya siasa vilivyobaki kuendelea kutekeleza matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa kama ilivyo, ili kuepuka kufutwa.

Aidha, natumia fursa hii vilevile kuviasa vyama vya siasa kuheshimu katiba na kanuni za vyama vyao, ili kuepusha migongano na migogoro ndani ya vyama, ambayo inafanya vyama kuwa dhaifu na kushindwa kutekeleza sheria na majukumu yake ya kisiasa ipasavyo.

 

Jaji Francis S.K. Mutungi

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

09 Novemba, 2016

                                                                   

 
 
Follow Us: