News

Shibuda Ataka Rais Magufuli Aungwe Mkono

2017-01-29 17:36:09

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John M. Shibuda i amewataka wananchi kumuunga mkono Rais wa awamu ya tano Mhe. John Pombe Magufuli kwa sababu anatekeleza mnyumbuliko wa uwajibikaji wa utawala Bora. 

Hayo yamesemwa leo wakati akitoa salamu za ujumbe maalum wa kumaliza salama mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017 mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es salaam

Shibuda amesema uwajibikaji umechangia ustawi na maendeleo ya nchi  pamoja na uishi hai wa vyama vya kisiasa katika awamu ya utumishi wa utawala wa awamu ya tano. 

Amempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wake wasaidizi wakuu ambao ni Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu, Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa na viongozi wote wanaombatana na Serikali ya awamu ya Tano.

Shibuda amesema kuwa Rais wa awamu ya tano , Mhe John Pombe Magufuli amekuwa na maono ya kuliweka taifa katika kuwa  na dira ya mpango mkakati wa kuwa na Serikali inayojitegemea,  kudhibiti matumizi hewa yasiyo na maslahi wala tija kwa taifa na pia kwa kuondoa upendelevu na matabaka. 

“Kwa umuhimu wa pekee napenda kufichua  angalizo la kwamba,Tanzania ya Serikali ya awamu ya Tano tuipongeze imetekeleza uvumbuzi ambao umekuwa ni tabibu kwa kasoro zilizokuwa ni hitilafu kwa Serikali ya CCM kuitwa ni Serikali ya watu wa Tanzania waliokombolewa na TANU na ASP” amesema Shibuda.

Amesema kulikuwa na kasoro zilizokuwa na hitilafu ambazo awamu ya Tano imedhibiti mirija ya unyonywaji wa pato la Taifa wa kupitia watumishi hewa, wanafunzi hewa, kaya za masikini Bandia na kupitia wahujumu uchumi wa matumizi mabaya ya dhamana za Taifa.

Shibuda amesema  Serikali ya awamu ya Tano imerejesha uhodari, uwajibikaji wa watumishi  na sasa  wamekuwa wana tabia za miiko ya utiifu kwa Umma.

Amesema sasa urasimu katika utolewaji wa huduma kwa mahitaji ya ustawi wa maendeleo ya Jamii ya Afya na Elimu na utatuzi wa kero kwa kasi ya kuwepo uishi wa Amani na furaha kwa makundi yote ya kijamii.

Aliongeza kuwa  uhuru wa nchi sasa umekuwa siyo wa kunufaisha tabaka maalum la Raia wa Tanzania ni watu wote wamekuwa wanufaika na uhuru wao katika nchi na maendeleo yanaonekana.

 

 

 
 
Follow Us: