Chama cha The Union for Multi-party Democracy of Tanzania, ambacho kwa kifupi kinajulikana kwa kutamkwa kwa herufi tatu UMD. Ni chama cha kisiasa kilichoanzishwa hapa nchini Tanzania mnamo mwaka 1992. Baada ya kurudishwa tena kwa mfumo wa siasa wa vyama vingi mnamo mwaka huohuo wa 1992 na kupata usajili wake wa kudumu mnamo tarehe 21/01/1993 na kukabidhiwa cheti cha usajili chenye namba 004/93 mikononi mwa mwasisi wa chama hicho hayati chifu Abdallah Saidi Fundikira. Chama cha UMD, ni chama kilichostawi kwa haraka sana nchini mwetu hasa ukizingatia umaarufu mkubwa wa mwasisi wake na uwerevu mkubwa wa kisiasa na uongozi, ilikuwa ni sifa moja kubwa iliyopelekea watu mbalimbali kuvutiwa na chama cha UMD. Chama cha UMD kilifanya mkutano wake mkuu wa kwanza wa kuchagua viongozi wake wa kitaifa, wa kukiongoza chama cha UMD kwa muda wa miaka mitano (5). Uchaguzi huo ulimpa fursa mwasisi wa chama hicho Chifu Abdallah Saidi Fundikira kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha UMD kwa kipindi cha miaka mitano (5). Ambapo mkutano huo mkuu ulifanyika mwaka 1994 katika ukumbi wa Technical College Dar Es Salaam. Katika uchaguzi huo miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wengine waliofanikiwa kuchaguliwa ni pamoja na ndugu Wilson Kawata aliyeshika nafasi ya katibu mkuu, ndugu Simon Kashura aliyechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti bara na wengine ni ndugu Salum Suleimani Ali aliyechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti Zanzibar na ndugu Idrisa Ali aliyekuwa naibu katibu mkuu Zanzibar. Kimsingi nguvu yenye uwezo mkubwa wa kufikiri, kupanga na kutekeleza mambo mengi makubwa na ya msingi kutoka kwa viongozi hao walikiwezesha chama chetu cha UMD kufanya vizuri katika chaguzi za awali ambazo chama chetu kiliamua kushiriki. Mfano wa kutizamwa ni pale katika chaguzi za serikali za mitaa, vijijini na vitongoji uliofanyika mwaka 1993, ambapo kiliweza kupata viti mia moja na kumi na moja (111) na kufuatiwa na chaguzi za madiwani. Pamoja na mfumo huo wa demokrasia ya vyama vingi kuogopwa na watawala, hofu iliyopelekea kuvisema vibaya vyama vya siasa kutokana na ugeni wa mfumo huo na kuvifanyia hila vyama vilivyokuwa vikionekana kuweza kufanya vizuri 2 kama chama cha UMD bado chama cha UMD kiliweza kupata madiwani watatu katika uchaguzi wa madiwani uliofanyika mwaka 1994. Chama chetu kilianza kufanya vibaya na kupoteza nguvu zake baada ya viongozi wa kitaifa wakiongozwa na mwasisi wetu Chifu Abdallah Saidi Fundikira kugomea na kutishia kuwa chama chetu hakitashiriki katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 1995 mpaka mabadiliko ya katiba yafanyike na nchi kupata katiba mpya. Na kupelekea kuanzishwa kwa kauli mbiu ya kitanda kwa kitanda mpaka katiba mpya ipatikane Jambo ambalo lilianza kuwagawa wanachama na kuleta mpasuko mkubwa wa kifikra kati ya viongozi waliokuwepo madarakani na wanachama, hadi kupelekea baadhi ya wanachama na viongozi wengine kuelekea katika vyama vingine. Pia hali iliendelea kuwa si shwari hata pale ambapo viongozi wakuu walipoleta tathmini zao na kutaka kufanyike juhudi za kukiokoa chama kisiangamie, bado viongozi wenyewe walihitilafiana kwa kugawanyika makundi mawili, ambapo wapo baadhi ya viongozi na wanachama waliokataa kushiriki kabisa katika uchaguzi na wapo baadhi ya viongozi na wanachama walioamua kushiriki katika uchaguzi kwa lengo la kukinusuru chama, jambo ambalo lilianza kupelekea kufanya vibaya kwa chama chetu katika uchaguzi huo mkuu uliofanyika mwaka 1995 na chaguzi za mbele zilizoendelea. Kazi kubwa inayoendelea kufanywa na viongozi waliopo madarakani hivi sasa ni kuendelea kujenga umoja na mshikamano ndani ya chama ili chama kiendelee kujengeka na hatimae kirudishe nguvu zake. Na chama, kwa jitihada za viongozi wake tayari kimeshaanza kujijenga vizuri katika baadhi ya maeneo na kuanza kufanya vizuri katika chaguzi ndogo zilizopita, ambazo zilizofanyika mwaka 2024. Mungu ibariki Afrika. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki UMD. Imeandaliwa na …………………………… KATIBU MKUU, UMD
UMD
Makao Makuu
Mtaa wa Kwambano
Tabata Chang’omb
S.L.P 61117
Dar es Salaam
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu
Nyumba Na. E/124
Amani Masumbani,
Shehia, Kilimahewa Bondeni.
Unguja
S.L.P 2499
Zanzibar
Simu Na. +255 7776 137077 DC ZNZ
+255 7777 96184 DSG ZNZ